MTOTO wa mwaka mmoja (jina linahifadhiwa) wa jijini Dar es Salaam amewahuzunisha wengi alipokutwa amekaa na maiti za wazazi wake chumbani, Uwazi limedokezwa.

Baba mzazi wa mtoto huyo aliyetambulika kwa jina moja Pascal (24) na mama yake, Rose Mary Gallus (34), wakazi wa Gongo la Mikongeni- Mboto jijini Dar, walikutwa wamekufa chumbani kwao wiki iliyopita.Chanzo kutoka eneo la tukio kililiambia Uwazi kuwa, tukio hilo lilijiri Novemba 19, mwaka huu ambapo miili ya watu hao ilikutwa sakafuni na majeraha ya visu.

“Damu zilikuwa zimetapakaa chumba kizima, huku yule mtoto naye akiwa amejeruhiwa kiasi na alikuwa amelowa damu.

“Ni tukio lililotushangaza, wengi walimhurumia sana yule mtoto kwa kuachwa yatima,” kilieleza chanzo chetu.CHANZO CHA MAUAJI NI NINI?

Pekuapekua ya wandishi wetu ilibaini kuwa, baba wa mtoto huyo ndiye chanzo cha vifo hivyo na kwamba alianza kumuua mkewe kwa visu kisha naye kujiua baadaye kwa kujichoma visu kifuani na tumboni.BABA WA ROSE MARY ASIMULIA

Akizungumza na Uwazi, baba mzazi wa marehemu Rose, Gallus Mwape alisema;

“Siku hiyo mwanangu alikuja asubuhi nyumbani kwangu, Gongo la Mboto, Mwisho, kumleta mjukuu wangu (mtoto wa mwaka mmoja) ambaye ni mtoto wake ili yeye aende kwenye shughuli zake kwa kuwa pale alipopanga hana mtu wa kumuachia mtoto.

“Ilipofika jioni akaja kumfuata mtoto na kurejea nyumbani kwake. Saa tatu kasoro usiku nilipigiwa simu na jirani yake mwanangu.“Akaniambia niende nyumbani kwa mwanangu kuna matatizo. Nilipofika pale nilikuta kuna kundi la watu, ikabidi nishtuke, nikajiuliza kuna nini tena kimetokea?

“Wazo la kuwa mwanangu ameuawa sikuwa nalo kabisa, ikabidi niingie ndani, nikakuta maiti zikiwa chini, damu imetapakaa chumba kizima.”Aliongeza kuwa, mwanaye huyo alikuwa akiishi peke yake na mwanaume aliyefanya tukio hilo la kinyama alikuwa akienda pale kama mzazi mwenzake kwa kuwa wanamtambua kama mkwe mtarajiwa ingawa hakuwa amefanya chochote kukamilisha masuala ya ndoa.YALIYOTOKEA ENEO LA TUKIO

Inaelezwa na vyanzo mbalimbali kuwa, siku hiyo ya tukio, majirani walimsikia Pascal akigombana na mkewe huku akimtuhumu kuwa si mwaminifu katika mapenzi.

Hata hivyo, majirani hawakutilia maanani wakiamini kuwa ugomvi huo utaisha kwa amani, jambo ambalo halikuwa hivyo.“Baada ya muda tukasikia vishindo ndani, sauti ya mtu kukoroma ikawa inasikika, ikabidi twende kwa mwenyekiti wa mtaa kumweleza.

“Alipofika mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, ikabidi kuuvunja kwa sababu hakuna aliyeitikia hodi ya mwenyekiti.“Tulipoingia ndani tukakuta Rose amekufa na mumewe pia huku mtoto wao akiwa amekaa anaangalia maiti za wazazi wake,” kilisema chanzo.

Chanzo kingine kiliongeza madai kuwa, Paschal ndiye aliyemuua mkewe na alipoona harakati za kuita polisi na mwenyekiti zinafanywa na majirani ndipo naye akaamua kujiua.HUYU HAPA KAMANDA WA POLISI

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, ACP Zuberi Chembera alisema kuwa, taarifa ya tukio hilo zimefika mezani kwake.

“Taarifa ya kijana huyo kumuua mpenzi wake na yeye kujiua ninazijua.“Kwa mujibu wa wazazi wa mwanamke; mwanaume anayetuhumiwa kuua alikuwa amezaa na mtoto wao na kwamba walikuwa wameachana kwa tabia za ukorofi wa kijana huyo.

“Siku hiyo ya tukio mwanaume huyo alikwenda kwa mwenzake lengo likiwa ni kusuluhisha dosari zao ili wafunge ndoa, ndiyo yakatokea mauaji hayo; nadhani baada ya mwafaka kati yao kushindikana,” alisema Kamanda Chembera.