ALIYEKUWA mkuu wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Peter Toima Kiroya anadaiwa kuburuzwa polisi na mkewe Philomena Toima kwa tuhuma za kumpiga na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.Akizungumza na UWAZI hivi karibuni, Philomena alidai chanzo cha ndoa yake kuingia shubiri ni kitendo cha mumewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa takriban miaka miwili sasa na mwanamke anayetambulika kwa jina la Scolla Mollel.Philomena alisema kwa kuwa Toima amekuwa na mahusiano ya muda mrefu na Scolla, hadi kufikia hatua ya kuhamia huko na kuishi na mwanamke huyo kama nyumba ndogo.“Alinipiga hadi nikakimbizwa hospitalini kupatiwa matibabu. Tayari suala hilo limesharipotiwa polisi katika kituo cha polisi cha Komolo Novemba 16 mwaka huu na kufungua jalada la shambulio nambari KML /RB /137/2019,” alisema.


Akifafanua kwa kina kuhusu tukio hilo, Philomena alidai kuwa Novemba 15 mwaka huu muda wa saa 12:30 jioni, wakiwa nyumbani kwao Komolo, kulitokea mabishano makali kuhusu uhusiano na tabia za mumewe kuchepuka nje ya ndoa.“Ndipo Toima alipochukua uwamuzi wa kunishushia kipigo, ikabidi nikimbilie katika kituo kidogo cha polisi cha Komolo kutafuta msaada,” alisema.

Philomena aliongeza kuwa mume wake amekuwa na hulka ya kumpiga, kumtishia kwa silaha, kumdhalilisha sanjari na kumtukana matusi ya nguoni.Aliongeza kuwa chanzo cha matatizo kwenye ndoa yao kilianza mwaka juzi baada ya mume wake kumwajiri Scolla kama mtunza fedha katika taasisi waliyoianzisha na mumewe ambayo inatambulika kwa jina la ECLAT Development Foundation.“Mara baada ya kubaini mume wangu ana uhusiano na mwanamke huyo, nilimuuliza kuhusu madai hayo lakini cha ajabu alimwondoa kazini na kwenda kumjengea nyumba ambayo wanaishi pamoja mpaka sasa.“Nilipobaini kwamba mume wangu ana uhusiano usiofaa na mwanamke huyo nilimfuata na kumweleza, lakini cha ajabu alimhamisha akawa anafanya shughuli za ofisi akiwa nyumbani alipomjengea” alisema Philomena

Hata hivyo, alisisitiza kuwa tangu mumewe aanze uhusiano huo na mwanamke huyo, ndoa yake imekosa amani huku mumewe akitumia rasilimali mbalimbali za taasisi yao kumfadhili mwanamke huyo.Alipotafutwa kwa njia ya simu, Toima alikanusha vikali madai yote na kusema kwamba suala hilo liko mikononi mwa wazee wa ukoo huku akisisitiza kwamba kumekuwa na watu wa pembeni walio karibu na mkewe wanaomrubuni na kumpotosha.

“Hilo suala litakuja kumletea shida kubwa huyu mwanamke kwa kuwa liko kwa wazee halafu kuna ndugu zake wanaompotosha” alisema Toima.Alipoulizwa kuhusu madai ya kumpiga mara kwa mara mkewe na kutumia hovyo rasilimali fedha za taasisi kwa kumpatia mwanamke huyo, alikanusha vikali na kusema kuwa kwa sasa yuko safarini nyanda za juu Kusini na pindi akirejea mkoani Arusha atafunguka kuhusu tukio zima.


Hata hivyo, alipotafutwa kwa mara nyingine baada ya kurejea safarini, aliendelea kukanusha madai hayo ya kumpiga mkewe na kushangaa taarifa za tukio hilo kuvuja kwenye vyombo vya habari.

Kwa upande wake mwanamke anayedaiwa kuvuruga ndoa ya wawili hao (Scolla) alipohojiwa alisema kwa kifupi kwamba endapo angekuwa anavuruga ndoa hiyo angeshafikishwa mbele ya vyombo vya dola vikiwemo polisi na kisha kukata simu.Hata hivyo, Scolla alikiri kumtambua Toima kama bosi wake na kudai kuwa mambo mengine yeye hayajui na kumhoji mwandishi wa habari hizi kwa kauli tata kuwa kwani yeye hafai kuwa mke?

Uwazi linaendelea kuchimbua zaidi habari hii, ikiwepo jitihada ya kufika nyumbani kwa msichana anayedaiwa kuchepuka na mkuu huyo wa wilaya mstaafu kwa kufanya uchunguzi wa kile kilichopo na baadaye kuanika ukweli mzima.