Jumla ya watahiniwa 485,866 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne (CSEE) utakaoanza kufanyila leo hadi Novemba 22, mwaka huu, huku idadi ya watahiniwa hao ikiongezeka kwa asilimia 1.37 ukilinganisha na mwaka jana.

Kati ya watahiniwa hao, watahiniwa wa shule ni 433,052 na wa kujitegemea ni 52,814 na kwamba idadi ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa mwaka jana ni 427,181, hivyo ni ongezeko la watahiniwa 5,871 kwa mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde alisema mtihani huo utafanywa katika jumla ya shule za sekondari 4,933 na kwenye vituo 1,050 vya watahiniwa wa kujitegemea.

Kati ya watahiniwa hao wa shule, wanaume ni 206,420 sawa na asilimia 47.67 na wanawake 226,632 sawa na asilimia 52.33.

Pia, watahiniwa wenye mahitaji maalumu wapo 842, kati yao 450 ni wenye uoni hafifu, 42 wasioona, 200 wenye ulemavu wa kusikia na 150 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,814 waliosajiliwa wanaume ni 23,418 sawa na asilimia 44.37 na wanawake ni 29,396 sawa na asilimia 55.66.

Kati yao watahiniwa hao wa kujitegemea wenye mahitaji maalum wako 28 ambapo wenye uoni hafifu ni 20 na wasioona wanane.