WIZARA ya afya Zanzibar imemsimamisha kazi daktari wa Hospitali ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba, Massoud Sleiman Abdalla, kutokana tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa mwanamke mjamzito.Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumanne, Novemba 26, 2019, Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed, amesema wamefanya hivyo kwa mujibu wa sheria.Amesema wamepokea barua kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (ZAECA) yenye maelezo kuhusu kukamatwa kwake hivyo wamelazimika kufuata taratibu za kazi ikiwemo kumsimamisha kazi.Amesema licha ya daktari huyo kukamatwa kwa tuhuma hizo haimaanishi kila mtaalamu wa afya ndiyo tabia zao kwani huenda wakawapo wachache wenye dhamira ya kuichafua kada hiyo.Awali, Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji wa wizara hiyo, Ramadhan Khamis Juma, amesema kwa kuwa mtuhumiwa amekamatwa kwa hatia hiyo hawana budi kufuata sheria za kazi.Amesema tayari wameshamwandikia na kumkabidhi barua mtuhumiwa huyo ya kusimamishwa kwake. Amesema kwa kuwa mtuhumiwa amesimamishwa kazi atalazimika kupokea nusu mshahara kwa kipindi cha miezi sita na baada ya hapo iwapo kesi yake itakuwa haijamalizika mshahara huo utasitishwa kabisa.