DAR: Kweli ushoga kazi! Staa wa filamu za Kibongo, Aunt Ezekiel amekubali kumpa staa mwenzake, Wema Isaac Sepetu, mwanaye Cookie aliyezaa na mpenzi wake, Moses Iyobo ‘Moze’.

Aunt ameliambia Gazeti la Ijumaa kuwa, amempa Wema mwanaye ili awe kama wa kwake maana yeye anatarajia kuzaa mwingine wa kiume hivi karibuni kwa majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.

Aunt alitaja sababu ya kumkabidhi Wema mtoto wake huyo kuwa walikubaliana hivyo tangu akiwa mjamzito. Alisema walikubaliana kuwa akijifungua tu, mtoto atakayezaliwa atakuwa ni wa Wema.

“Unajua hata kama nitajibaraguza vipi, lakini ukweli ni kwamba nilimuahidi shoga yangu Wema kumpa mtoto ambaye nitamzaa, ukizingatia alikuwa na mimi bega kwa bega hadi wakati ninajifungua na baada ya kujifungua,” alisema Aunt ambaye amekuwa na urafiki wa miaka kadhaa na Wema.

Kwa upande wa Wema alipozungumzia ishu hiyo na Gazeti la Ijumaa, Wema alisema ni ahadi waliyowekeana katika urafiki wao huo na kwa vile ana uhitaji mkubwa wa mtoto, atafanya hivyo, yaani kumpokea mtoto huyo kwa mikono yote kutoka kwa Wema.

“Huyu Cookie ni wangu tulishakubaliana kitambo na yeye alisema kwa kinywa chake mwenyewe kuhusu kunipa mtoto tangu alipokuwa mjamzito na mimi ninamchukua kama mtoto wangu,” alisema Wema ambaye amekuwa akililia kupata mtoto.