HUKO mitandaoni kumechafuka! Watu wanajadili hayo magari mapya mawili ambayo mwigizaji Wema Isaac Sepetu, wengi waliamini alizawadiwa kwenye bethidei yake, lakini wakati huohuo, zengwe limeibuka kuhusu magari hayo, Gazeti la Ijumaa Wikienda lina mchezo mzima.

Mrembo huyo mwenye nyota ya kupendwa tangu alipotwaa Taji la Miss Tanzania 2006 hadi leo, aliichafua mitandao ya kijamii hususan Instagram kuanzia Alhamisi iliyopita na mambo yakawa moto zaidi siku ya kilele (Ijumaa) baada ya kufanya bonge moja la pati ndani ya kiota cha Elements, Masaki jijini Dar.NDINGA ZENYEWE

Wakati watu wakiendelea kumpongeza kwenye mitandao ya kijamii usiku huo, baadhi ya watu walitumia nafasi hiyohiyo kumpongeza Wema kwani tayari yalitupiwa magari hayo mawili ambayo ilisemekana amezawadiwa.Magari hayo yalikuwa ni Toyota Crown na Toyota Vanguard. Toyota Crown iliyokuwa imepaki nje ya Ukumbi wa Elements, wananzengo walishindwa kung’amua ni nani aliyemzawadia zaidi tu ya kumuona Wema amefika kwenye gari hilo na kulithaminisha.

Habari ambazo hazijathibitishwa popote ni kwamba gari hilo alizawadiwa na ‘future husband’ wake wa sasa. Lakini Toyota Vanguard la rangi nyekundu kama lile la Hamisa Mobeto, hilo wananzengo walijiongeza kwa kusema amezawadiwa na shosti wake wa muda wote, mwigizaji Aunt Ezekiel kwa kuwa ndiye aliyetinga nalo ukumbini hapo na Wema kwenda kumlaki.ZENGWE SASA…

Wakati shamrashamra zikiendelea ukumbini, wananzengo hawakungoja kukuche. Usiku huohuo wakalieleza Gazet la Ijumaa Wikienda kuhusu utata wanaouona katika magari ambayo yamefikishwa ukimbini hapo ikiaminika ni zawadi alizopewa mrembo huyo.“Si bure hapa nahisi kuna mchezo unachezwa, mbona hili gari Vanguard lenyewe hatumuoni hata huyo aliyemtunza? Inawezekanaje tu Wema aletewe gari halafu aliyemletea tusimuone?” Alihoji mwananzengo mmoja aliyekuwepo ukumbini aliyejitambulisha kwa jina moja la Kitalii.

WADAU WAPINGA…

Gazeti la Ijumaa Wikienda pia lilizungumza na wadau wengine tofautitofauti ambao walikwenda mbali zaidi kwa kueleza kwamba wana shaka na magari hayo kwani mbali na hilo ambalo halijulikani lililetwa na nani, hata hilo alilokuja nalo Aunt pia lina viashiria vya utata.“Jamani…jamani hivi kweli kwa usawa huu Aunt anaweza kweli kumnunulia gari Wema? Sawa ni marafiki, lakini ukitazama lile gari alilonunua halafu ukiangalia na gari analomiliki yeye ni vitu viwili tofauti. Haiwezekani ampe mwenzake gari la thamani halafu yeye ana gari la kawaida,” alisikika mmoja wa wadau wakubwa wa burudani ambaye aliomba hifadhi ya jina.Ijumaa Wikienda linafahamu kuwa Aunt kwa sasa anamiliki gari aina ya Toyota Porte, lakini huko nyuma aliwahi kuwa na Toyota Alphard ambalo kwa sasa haonekani nalo tena.

JIPU PWAA!

Kufuatia minong’ono kuwa mingi kuhusu utata wa magari hayo, Ijumaa Wikienda lililazimika kumfikia Aunt ambaye alitegua kitendawili kuhusu gari ambalo wengi walifikiri amemzawadia Wema.“Hili gari ni langu jamani, nimejizawadia mwenyewe kwani bethidei yangu inakaribia hivyo niliona nijinunulie zawadi mapema kabisa. “Kinachonishangaza watu wanapenda tu kujiongeza bila hata kujua ukweli wa mambo, nimeona huko mitandaoni wanasema eti nimemzawadia Wema wakati si kweli.“Hapa tumekuja kwenye sherehe kula bata na kufurahia kwa pamoja na rafiki yetu kipenzi cha Watanzania, ameongeza mwaka mwingine wa kuishi hapa duniani,” alisema Aunt. Alipoulizwa kuhusu gari lingine aina ya Toyota Crown, Aunt alisema hilo hawezi kulizungumzia kwa sababu shosti yake huyo hajamueleza chochote naye ameliona tu palepale.

WEMA UBIZE KAMA WOTE

Jitihada za kuzungumza na Wema usiku huo hazikuzaa matunda kufuatia kuwa bize na sherehe, lakini hata hivyo, Ijumaa Wikienda bado lipo mzigoni kulifuatilia gari hilo aina ya Toyota Crown ambalo mitandaoni ilidaiwa mrembo huyo amezawadiwa kwenye sherehe yake hiyo ya kuzaliwa.Hata hivyo, kwenye sherehe za kuzaliwa, Wema kujizawadia gari pia inawezekana. Aliwahi kufanya hivyo mwaka 2015 katika Ukumbi wa Millenium Towers, Kijitonyama jijini Dar ambapo aliwatoa wageni waalikwa hadi nje ya ukumbi huo na kuwaonesha gari aina ya Range Rover Evogue ambalo alidai amejizawadia. Mwanadada huyo alisema gari hilo alilinunua kwa thamani ya shilingi milioni 140 Kibongo.