Mashambulizi ya angani yamepiga maeneo ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran karibu na mpaka wa Syria na Iraq kulingana na wanaharakati.

Shirika la haki za kibinadamu la Syrian Observatory for Human Rights, lililo na makao yake nchini Uingereza limesema kwamba takriban wapiganaji 18 wa Iran na wale wanaoungwa mkono na Iran waliuawa.

Haijulikani ni nani aliyetekeleza mashambulio hayo usiku kucha ndani na nje ya mji wa Albu kamal.

Lakini Israel imetekeleza mamia ya mashambulizi dhidi ya kambi za Iran nchini Syria wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Lengo la Israel ni kuangamiza kile inachokitaja kuwa uwezo wa kijeshi wa Iran nchini Syria mbali na usafirishaji wa silaha za Iran kwa makundi ya kijeshi kama vile Hezbollah nchini Lebanon.

Shirika hilo la haki za kibinadamu lilinukuu vyanzo vyake vikisema kwamba ndege hizo zisizojulikana zililipua kambi na hifadhi za zana na magari yanayomilikiwa na wapiganaji wa Iran katika eneo la al- Hizam al-Akhdar pamoja na maeneo mengine karibu na Albu Kamal.

Omar Abu Layla , mwanaharakati mwenye makao yake Ulaya kutoka kundi la DeirEzzor 24 , alisema kwamba milipuko mikubwa ilisikika katika mji huo na kwamba kulikuwa na ghasia na hofu miongoni mwa wapiganaji hao.

Kundi jingine kwa jina Sound and Pictures , lilinukuu maafisa wa afya waliosema kwamba takriban watu 21 waliuawa na kwamba wapiganaji walichukua mifuko yote ya damu katika hospitali ya Albu kamal ili kuwapona wapiganaji wao waliojeruhiwa'