Msanii wa muziki wa kizazi kipya Ommy Dimpozi akifuta machozi wakati akitoa burudani kwenye jukwaa la Tigo Fiesta katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza

TAMASHA la Muziki, Msimu wa Tigo Fiesta 2019 limezinduliwa jana kwa kishindo jijini Mwanza huku kundi la Weusi likifunika kwa kuwapagawisha washabiki luluki waliojitokeza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.Mbali na wasanii hao kukonga vilivyo nyoyo za washabiki wa muziki wa kizazi kipya msanii mwingine machachari Farid Kubanda ‘Fid Q’ hakuwa nyuma kuwarusha wapenzi  huku Omar maarufu kama Ommy Dimpoz akimwaga kukwaani.Washabiki waliojitokeza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba walishindwa kujizuia kutokana na makamuzi ya nguvu yaliyowaacha hoi yaliyofanywa na kundi la Weusi wakiongozwa na JOH Makini,Nikki wa pili na G Nako baada ya  kupanda jukwaani na kutoa burudani tosha.


Aidha, katika tamasha hilo la Tigo Fiesta 2019 msanii Fid Q alipanda jukwaani akiwa kwenye Wheel Chair (kiti cha magurudumu mawili) kabla ya  kuwazodoa waliomzushia kifo na kwamba hataweza kuimba kutokana na kuugua maradhi kwenye koo kasha kumwaga machozi mithili ya mtoto.


Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Weusi  wakishambulia jukwaa la Tigo Fiesta

Tamasha hilo limefanyika Mwanza kwa mara ya kwanza kuasisiwa kwake lilikuwa na mvuto na msisimko mkubwa ambapo washabiki kutoka viunga vya jiji hilo la  milima ya miamba ya mawe  walisuuzika nyoyo na mara kadhaa walishiriki kuimba nyimbo za wasanii mbalimbali hasa kundi la Weusi na Fid Q.


Mkali wa HipHop  Fareed Kubanda ”Fid Q” akitoa burudani kwenye jukwaa la Tigo Fiesta

Mbali na kundi la weusi lililopagawisha vilivyo, wengine ni Barnaba, TID, Mavoko na Diva ambapo wasanii wa jiji la Mwanza nao hawakubaki nyuma.Akizindua tamasha hilo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela alisema waandaaji wa Tigo Fiesta 2019 kwa ubunifu na uamuzi wao wa kuzindua tamasha hilo hawakukosea ikizingatiwa jiji hilo ni kitovu cha biashara kwa nchi  za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati.


Lulu Diva akitawala jukwaa la Tigo Fiesta 2019

“Mwanza ni kisima cha burudani kutoka na kuwa na wapenzi wengi wa muziki wa kizazi kipya hivyo niwapongeze Clouds na Tigo kwa ubunifu wao wa kuandaa na kuzindua tamasha lao hapa.Sisi kama mkoa tutaendelea kuwaunga mkono.“Pia  tamasha hili mbali na kutoa burudani lina umuhimu kiuchumi, linatoa ajira za muda mfupi,linaongeza kipato cha wananchi wetu na waandaaji nao wananufaika,”alisema Mongela.Kwa upande wake Mkurugenzi wa Clouds Media Entertainment, Joseph Kusaga, alisema wana mapenzi nakubwa na Mkoa wa Mwanza na  ndiyo sababu  msimu huu wamezindua tamasha la Tigo Fiesta 2019 kwa kutambua mchango wa mkoa huo.


TID ” Mnyama” akipagawisha jukwaa la Tigo Fiesta 2019

Naye Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Ziwa, Uthmaan Madati, kampuni hiyo ya mawasiliano itaendelea kushirikiana na kuiunga mkono Clouds  ili kuhakikisha wanawapatia Watanzania burudani yenye vionjo na ladha tofauti tofauti.Hata hivyo washabiki na wapenzi Tigo Fiesta 2019 waligubikwa na huzuni na simanzi ya muda mfupi wakati  kundi la wasanii wa Tanzania House of Talent (THT) likitoa  burudani huku wakionyesha picha za aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds, marehemu Ruge Mutahaba ikiwa ishara ya kumbukumbu yake.


Nandy ; African Princess” akishambulia jukwaa la Tigo Fiesta 2019 _Saizi yako katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza

Ikumbukwe marehemu Ruge kabla ya kufikwa na mauti alikuwa mhimili na muasisi wa tamasha hilo zamani likiitwa Fiesta kabla ya kubadilishwa na kuitwa Tigo Fiesta. Tamasha hilo baada ya kuzinduliwa mashambulizi yataelekezwa mkoani Kagera katika Wilaya ya Muleba na hivyo wapenzi wa huko wakae mkao wa kula kwa nafasi.