Msanii maarufu kutoka nchini Tanzania, Harmonize, kwa sasa ameaga ukapera rasmi baada ya kufunga pinga za maisha katika hafla ya kisiri iliyoandaliwa siku ya Jumamosi, Aprili 7. Mwimbaji huyo wa wimbo tajika Kwangwaru, alifanya harusi na mpenzi wake wa muda mrefu mzaliwa wa Italia, Sarah Michelotti, kwenye hafla iliyohudhuriwa na jamaa na marafiki.

Kupitia kwa video iliyobainishwa na TUKO.co.ke, inamuonyesha Harmonize na mkewe Sarah wakifurahia moja kati ya nyimbo zake huku wakishangiliwa na wageni wao. Hii ilitamatisha vyema safari ya mapenzi ya Harmonize, ambaye amekuwa akichumbiana na mrembo huyo tangu alipoanza kuwa maarufu.

Mwanamuziki huyo alimchumbia mrembo huyo wa Italia mnamo mwezi Aprili 2019 baada ya kuwa kwenye uhusiano kwa miaka miwili. Fununu kuhusu uwezekano wa wawili hao kutengana ulianza kuenea mwaka 2018 wakati mashabiki kutambua kuwa wapenzi hao hawakuwa wakitumia muda wao pamoja huku Harmonize akihusishwa na mpenzi wake wa zamani Jacqueline Wolper.