MTOTO aliyejipatia ustaa kupitia mitandao ya kijamii, Maisara Mohammed ‘Mai Zumo’ (5), nyota yake imezidi kung’ara baada ya wiki iliyopita kukutana uso kwa uso na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa.Mai alianza kuwika baada ya kuwa anarekodiwa video za vichekesho na kupostiwa kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo hivi karibuni alikutana na Waziri Mkuu katika maadhimisho ya Siku ya Kunywa Maziwa Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Iringa.Katika mahojiano na Gazeti la Ijumaa Wikienda, baba mzazi wa mtoto huyo, Mohammed Kingara ‘Anko Zumo’ ambaye amekuwa ‘akim-brandi’ binti yake huyo alisema kuwa alifurahi mno mwanaye huyo kukutana na Waziri Mkuu.Anasema ilikuwa ni siku nzuri mno kwa Mai hivyo anaamini kwamba ndoto za mwanaye huyo zinazidi kutimia.

“Kwenye tukio lile Waziri Mkuu ndiye alikuwa mgeni rasmi na Mai naye alikuwepo kama balozi mkuu wa maziwa kwa watoto wenzake.“Hivyo Waziri Mkuu alipomuona Mai alisema alifurahi sana kukutana naye, lakini akaomba aanze kwanza kuongea na wananchi kabla ya kuzungumza na Mai kwa kuogopa kuchekeshwa.

“Kweli, baada Waziri Mkuu kumaliza kuzungumza na wananchi ndipo yeye na mke wake wakamuita Mai na kuanza kuzungumza naye, jambo ambalo kila mmoja lilimfurahisha.“Baada ya hapo tulirudi kukaa, lakini baadaye Waziri Mkuu alituita tena jukwaani na kututambulisha kama sisi ni mabalozi wa maziwa hivyo kututaka tuzidi kuhamasisha watu kunywa maziwa kwa wingi kwa sababu kauli mbiu yetu ni glasi moja ya maziwa kila siku kwa afya na elimu bora,” alisema.Anko Zumo anaendelea kusema kuwa, Waziri Mkuu hakumuahidi kitu chochote binti yake zaidi ya kufurahi kumuona na kumpa fedha taslimu.

“Kiukweli Waziri Mkuu hakumuahidi chochote zaidi ya kumpa zawadi ya fedha taslimu ambazo siwezi kutaja ilikuwa ni kiasi gani.

Kwa upande wake Mai mbele ya Waziri Mkuu alisema;

“Ninawashauri watoto wenzangu wanywe maziwa kwa afya zaidi.”