MATAJIRI wa Yanga jana wametimiza ahadi yao ya kuwapatia wachezaji wa Yanga milioni 50, baada ya kuwaondosha Township Rollers ya nchini Botswana, lakini wakiwaeleza kuwa wawaue na Zesco sasa.

Yanga imepangwa kuvaana na Zesco katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mchezo uliopangwa kuchezwa Septemba 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Championi Jumatano, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Saad Kimji alisema fedha hizo atakabidhiwa mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh kwa ajili ya kuziwasilisha kwa wachezaji ambao watagawana.
“Kabla ya mchezo wetu na Rollers, uongozi ulifanya kikao na wachezaji na kikubwa tulitaka kuona timu ikipata ushindi wa ugenini baada ya nyumbani kupata sare ya bao 1-1.


“Tunashukuru wachezaji waliwaondoa Rollers kwa kuwafunga nyumbani, hivyo kama uongozi tumeona tutimize hilo kwa kuwapatia fedha hizo.
“Hivyo, wakati wowote wachezaji hao watapatiwa fedha hizo na mratibu wa timu, tunataka kuona timu yetu ikisonga mbele katika michuano hiyo kwa kuwaondoa Zesco ambapo labda mambo yanaweza kuwa mengine,” alisema.

Juma Balinya ni mchezaji ambaye aliwawezesha wachezaji wa timu hiyo kupata fedha hizo baada ya kufunga bao pekee ugenini. Hapa nyumbani ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, bao la Yanga lilifungwa na Patrick Sibomana kwa mkwaju wa penalti