Jumba la kwanza la maonyesho duniani linalonuiwa kuonyesha kuhusu sehemu nyeti ya uke linatarajiwa kufunguliwa Uingereza.

Vagina Museum linalotarajiwa kufunguliwa mjini London litazinduliwa rasmi kwa mara ya kwanza November 16 kufuatia kampeni ya kuchangisha £50,000 kutoka kwa umma.

Jumba hilo linatarajiwa kuelimisha na kutoa uhamasisho kuhusu sehemu hiyo nyeti ya mwanamke na afya ya uke na pia kukabiliana na unyanyapaa.

Muasisi wake analitaja jumba hilo kama " jumba la kwanza duniani linalolenga kuangazia umbo la mwanamke."


Jumba hilo litaangazia maonyesho ya sanaa, michezo ya kuigiza, warsha na pia vichekesho, vyote vikiwa ni kuangazia kuhusu uke.

Mkurugenzi Florence Schechter aliamua kuliidhinisha jengo hilo la maonyesho mnamo 2017 baada ya kugundua Jumba la Phallological lililopo nchini Iceland, linaloonyesha kwa ukubwa uume, na kukosa kujumuisha sehemu hiyo nyeti ya umbo la mwanamke.

Amesema lengo la kufunguliwa jumba hilo la maonyesho London ni "kufuta unyanyapaa kuhusu mwili na umbo la mwanamke" kwa kila mtu haijalishi asili, jinsia au mahusiano.


Bi Schechter amesema jumba hilo ambalo ni la kitamaduni litaendesha miradi kwa watoto katika familia na pia shuleni.

Litaendehsa harakati za kuhakikisha watoto wanajihisi sawa kuzungumzia kuhusu sehemu hiyo nyeti ya mwanamke kuanzia umri mdogo.

"Wanapohisi aibu, inakuwa vigumu kuzungumzia mambo," amesema. "Ni kuhusu kuondoa unyanyapaa kutoka sehemu hiyo ya mwili na kuwa wakweli kuhusu kazi yake."