Mbunge wa Mbeya mjini (CHADEMA) ambaye pia ni msanii mkongwe wa 'HipHop' nchini Joseph Mbilinyi almaarufu 'Sugu' ametangaza kuacha muziki muda mfupi ujao.


Sugu ameandika kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Instagram kuwa muziki umemtoa mbali hadi kufika hapo alipo lakini umri na majukumu vinapelekea yeye kuweka 'mic' chini.

"Nimefanya muziki kwa miaka mingi sana sasa, nakiri umenitoa mbali sana nami nimeutoa mbali mpaka hapa ulipofika na mchango wangu kwenye GAME la Bongo na African Hip-hop si haba. Lakini kuliko kuwa kimya bila kuwa 'active' kimuziki nadhani sasa nalazimika kufikia mwisho na soon nitaweka rasmi mic chini", ameandika Sugu.

Ameendelea kuwa, "umri nao unasonga na majukumu mengine yanayohitaji muda wangu zaidi yanaendelea kuongezeka kwa neema zake Mungu lakini suala ni mashabiki wangu nawaagaje wakati utakapofika? Kwa albam au tamasha?".

Inawezekana Sugu akawa ndiye msanii wa kizazi kipya mwenye album nyingi. Mpaka sasa ametoa album takribani tisa. Album hizi ni kama “Ni Mimi” iliyotoka mwaka 1995, Ndani ya Bongo (1996), Niite Mr II (1998), Nje ya Bongo (1999), Millennium (2000), Muziki na Maisha (2001), Itikadi (2002), Sugu (2004), Coming of Age-Ujio Wa Umri (2006) na VETO iliyotoka mwaka 2009.