Shirikisho la mchezo wa mpira wa miguu duniani (FIFA) linazidi kudhihirisha kuwa halitaki utani wala madudu katika mchezo huo, FIFA wameonesha hayo kwa vitendo baada ya kushuhudia baadhi ya watu wakipoteza nafasi zao uongozi kutokana na kukumbwa na hatia ya makosa Fulani.

Kutokana na uchunguzi wao na kujiridhisha FIFA imetangaza rasmi kumfungia aliyekuwa Rais wa zamani wa chama cha soka cha Sudan Kusini Chabour Goc Alei kujihusisha na soka kwa miaka 10.

Kando na adhabu ya kufungiwa ambayo imeanza mara moja,pia amepigwa faini ya Dola 499,000 ( Tsh Bilioni 1.1) .
Chabour Goc Alei amepata adhabu hizo baada ya kukutwa na hatia ya makosa manne ambayo ni kubainika kuwa mpokea rushwa, mpokea tip (pesa ambazo zinalenga kukushawishi kufanya kitu), matumizi mabaya ya madaraka pamoja na matumizi mabaya ya fedha za taasisi hiyo.

Uchunguzi wa Ubadhirifu wa fedha umefanyika kuhusiana na hela ambazo chama cha soka cha Sudan Kusini kilipokea kutoka FIFA mwaka 2014 na 2015.